PAROKO wa Kanisa Katoliki, Parokia ya Epifania Kijichi, Dar es Salaam,
Respis Mzena, amehoji matukio ya watu wengi hasa wanasiasa kufa katika
kipindi hiki cha Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu kama ni mapenzi ya Mungu.
Paroko huyo alihoji hayo wakati akiongoza ibada ya kuaga mwili wa
aliyekuwa mgombea ubunge wa Jimbo la Ludewa, Deo Filikunjombe na wenzake
wawili, waliokufa katika ajali ya helikopta iliyotokea Alhamisi jioni
katika Pori la Akiba la Selous.
Mbali na marehemu Filikunjombe, wengine waliopoteza maisha na kuagwa
pamoja ni Plasdus Haule na Egid Nkwera ambao walikuwa watu wake wa
karibu.
Mwingine aliyepoteza maisha katika ajali hiyo ni rubani wa helikopta
hiyo, Kapteni William Silaa, ambaye ni baba mzazi wa Meya wa Manispaa ya
Ilala anayemaliza muda wake Jerry Silaa.
Akitoa mahubiri katika ibada ya kumuombea marehemu, Paroko huyo alisema
matukio ya vifo vya wanasiasa mwaka huu yanashangaza sana.
“Uchaguzi wa mwaka huu kuna nini hasa? kipindi hiki watu wanakufa sana
kila siku huyu kafa huyu kafa…kwanini watu wanakufa sana? Hii ni mipango
ya Mungu kweli?” alihoji Paroko huyo.
Akimuongelea marehemu Filikunjombe, alisema ni mtu aliyekuwa akijali na
kupenda watu wote ambapo alitoa maisha yake katika kutumikia watu bila
kujali itikadi zao.
Paroko huyo ambaye alisoma na Filikunjombe Seminari, alisema Serikali
ingekuwa na wabunge wachapakazi 30 kama alivyokuwa Filikunjombe, nchi
ingepiga hatua kubwa kwa sababu wakati wote alionekana akiwa jimboni
kwake akisaidiana na wananchi katika shughuli mbalimbali.
Awali viongozi mbalimbali na wananchi wakiongozwa na Rais Jakaya Kikwete waliaga miili ya marehemu hao.
Akisoma salamu za rambirambi kutoka kambi rasmi ya upinzani, mgombea
ubunge wa Jimbo la Kigoma Kusini kupitia NCCR-Mageuzi, David Kafulila
alisema taifa limepoteza mbunge wa mfano.
Akitoa salamu kutoka CCM, Mbunge wa Bumbuli ambaye anatetea nafasi yake,
January Makamba alisema chama kimepokea msiba huo kwa masikitiko
makubwa na kimepoteza kiongozi ambaye kwa kauli zake na vitendo,
aliwakumbusha nini hasa namna ya kuwa kiongozi wa CCM na kuwa mwana CCM.
Spika wa Bunge, Anne Makinda akitoa salamu za rambirambi kutoka bungeni,
alisema Filikunjombe alikuwa mfano wa kuigwa kwa vijana wote pamoja na
kuwa bungeni kwa miaka mitano lakini mambo aliyoyafanya ni kama mtu
aliyekaa zaidi ya miaka 20.
HABARI LEO


Post a Comment