SAFARI ya aliyekuwa mbunge mahiri wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Deo
Filikunjombe, hapa duniani, ilikamilika jana saa 10.30 jioni wakati
mwili wake ulipozikwa kwenye makaburi ya Kanisa Katoliki mjini Ludewa,
katika jimbo ambalo aliliongoza kwa ufanisi mkubwa kwa miaka mitano
iliyopita.
Vilio, huzuni, simanzi vilitawala wakati wa maziko ya mwanasiasa huyo
kijana ambaye alizikwa pamoja na wenzake wawili wanaotajwa kwamba
walikuwa watu wake wa karibu. Filikunjombe (43) aliyeiongoza Ludewa
kuanzia mwaka 2010 hadi Agosti mwaka huu, na aliyekuwa akitetea kiti
chake katika Uchaguzi Mkuu wa Jumapili wiki hii, alikufa katika ajali ya
helikopta iliyotokea Alhamisi wiki iliyopita baada ya kuanguka kwenye
Pori la Akiba la Selous mkoani Morogoro akitokea Dar es Saaam kwenda
Ludewa.
Spika Anne Makinda aliongoza mamia ya wananchi wa Ludewa waliojitokeza
kumzika mpendwa wao huyo, pamoja na wenzake wawili, Egid Nkwera (43) na
Cansablanca Haule (53), waliokufa pamoja katika ajali ya helikopta yenye
usajili wa namba 5Y-DDK ambayo pia ilichukua uhai wa rubani wake,
Kapteni William Silaa ambaye ni baba wa Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM,
Jerry Silaa.
Jerry pia ni mgombea ubunge wa CCM katika Jimbo la Ukonga mkoani Dar es
Salaam na alikuwa Meya wa Manispaa ya Ilala katika uongozi uliomalizika
hivi karibuni. Baba yake alitarajiwa kuzikwa jana jijini.
Filikunjombe na wenzake walizikwa saa 10.30 jioni katika makaburi ya
Kanisa Katoliki, ambako Askofu wa Jimbo Katoliki Njombe, Alfred Maluma,
aliendesha misa ya maziko, huku akiwataka wana Ludewa na familia kujipa
moyo na kumwomba Mungu awasaidie katika kipindi hiki kigumu cha
kuondokewa na wapendwa wao.
Akimzungumzia Filikunjombe, Spika Makinda alisema alikuwa ni nyota
ambayo ilianza kung’ara, alikuwa kijana mdogo aliyekuwa anawapenda
wananchi wake wa Ludewa na Taifa kwa ujumla katika utumishi wake wa
uwakilishi bungeni.
Makinda alisema anatamani kama Filikunjombe angeongoza wananchi wake kwa
miaka 20 zaidi kama yeye alivyoongoza Jimbo la Njombe Kusini ili
kukamilisha mipango yake kuwaletea maendeleo wa wananchi.
Viongozi wengine wa kitaifa waliohudhuria maziko hayo ni Makamu
Mwenyekiti wa CCM Bara, Philip Mangula, Kiongozi Mkuu wa Chama cha
ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya
Makazi, William Lukuvi na Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro
Nyalandu.
Akitoa salamu zake, Zitto alisema wananchi wa Ludewa ni vigumu kumpata
kiongozi wa aina ya Filikunjombe ambaye alikuwa mstari wa mbele kutetea
maslahi ya wananchi bila kujali itikadi za vyama vyao.
Filikunjombe na Zitto walijipatia umaarufu wakati wa sakata la Escrow
mwishoni mwa mwaka jana, Zitto akiwa Mwenyekiti wa PAC huku Filikunjombe
akiwa Makamu wake, kutokana na msimamo wao wa kutaka wahusika wote wa
kashfa hiyo iliyohusisha uchotwaji wa Sh bilioni 306, wachukuliwe hatua.
HABARI LEO


Post a Comment