Moshi. Vijana 50 wanaosadikiwa kuwa
ni wafuasi wa Chadema, wanadaiwa kufanya fujo kwenye mkutano wa hadhara
wa mgombea wa ubunge wa CCM katika Jimbo la Moshi Mjini, Davis Mosha na
kusababisha polisi wawatawanye kwa mabomu ya machozi.
Kamanda wa polisi mkoani Kilimanjaro, Fulgence Ngonyani alisema tukio
hilo lilitokea juzi katika eneo la Rau Madukani, Manispaa ya Moshi
mkoani Kilimanjaro.
Alisema mgombea wa CCM akiwa anatarajia kuzungumza na wanachi katika
eneo hilo, kulitokea kundi la vijana wanaokadiriwa kufikia 50 wakiwa na
silaha za jadi, marungu, mawe na fimbo na kuanza kuwashambulia watu
waliokuwa katika mkutano wa mgombea huyo.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Chadema katika Manispaa ya Moshi, Jafari
Michael ambaye pia ni mgombea ubunge, alikanusha vijana wa Chadema
kufanya vurugu hizo, bali alidai zilifanywa na vijana ambao hawajulikani
wana itikadi ya vyama gani.
Michael alivilaumu vyombo vya dola kuwa vinawapendelea CCM kiasi cha kila jambo likifanyika huwatuhumu vijana wa Chadema.
“Hata tukipeleka malalamiko polisi hawatusikilizi na hata kama vurugu
zikifanywa na wafuasi wa CCM wanasema ni Chadema, wanatuonea sana hawa
jamaa,” alilalamika Michael.
Alisema vijana waliokamatwa mtu hawezi kuwatuhumu moja kwa moja kuwa ni wa Chadema, kwa kuwa hawajulikani itikadi zao.
Kamanda Ngonyaji alidai kuwa chanzo cha vurugu hizo ni baada ya wafuasi
wa CCM kudaiwa kushusha bendera za Chadema zilizokuwa zimesimikwa
uwanjani hapo.
Alisema vurugu hizo zilisababisha majeruhi wawili aliowataja kuwa Wilson
Fabian (23) aliyepigwa jiwe kwenye paji la uso pamoja na mkono wa
kulia, mwingine hakufahamika jina mara moja na wote walipatiwa matibabu
katika Hospitali ya Mkoa ya Mawenzi.
Ngonyani alidai kuwa vurugu hizo zilisababisha uharibifu wa magari yaliyokuwapo uwanjani hapo baada ya kuvunjwa vioo.
Alisema watu kumi na moja wanashikiliwa kwa mahojiano kutokana na vurugu hizo kabla ya kufikishwa mahakamani kujibu mashtaka.
MWANANCHI


Post a Comment