
MWANANCHI
Kamati ya Maadili na Usalama ya CCM 
itakutana kesho mjini Dodoma kuanza shughuli yake ya kupitia taarifa za 
wagombea 38 wanaoomba kuwania urais na kisha kuwasilisha ushauri wake 
kwenye kikao cha Kamati Kuu inayokutana keshokutwa.
Habari kutoka ndani ya CCM zinasema kuwa kamati hiyo inayoongozwa na mwenyekiti wa chama hicho, Rais Jakaya Kikwete wakati mwingine hukasimisha shughuli zake kwa kamati ndogo inayoketi chini ya Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, Philip Mangula.
Mangula amekaririwa mara kadhaa akisema 
chama hicho kitatumia vigezo 13 vilivyowekwa na chama kuwachuja wagombea
 hao, akisisitiza kuwa watateua mgombea mwadilifu, mwenye uzoefu na 
atakayeuzika kwa wananchi.
Baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo walioko
 tayari mjini hapa kwa kazi hiyo walilieleza gazeti hili kuwa jukumu 
kubwa la kamati hiyo ni kuishauri Kamati Kuu juu ya masuala yote 
yanayohusu maadili ya wanachama na wagombea wa nafasi mbali ndani ya 
chama na kwenye vyombo vya Dola.
Mjumbe mmoja ambaye hakutaka jina lake 
litajwe gazetini kwa kuwa si msemaji alieleza kuwa kama kuna jambo 
kubwa, kamati ndogo huwa haikutani, badala yake kamati kubwa ikiwa chini
 ya Rais ndiyo hukutana na kuandaa taarifa za kuwasilisha kwenye Kamati 
Kuu.
Alitolea mfano wa mambo makubwa kuwa ni 
kama vile kupitia majina ya wanaowania kuteuliwa kugombea urais, kwamba 
kazi ya kamati ni kueleza taarifa za kila mwombaji, mazuri yake, mabaya 
yake na ushauri inaoutoa kwa wajumbe wa Kamati Kuu.
Mjumbe huyo alisema, Kamati ya Maadili 
na Usalama haina mamlaka ya kukata au kuongeza majina ya wagombea na 
kwamba mambo yanayopelekwa kwenye Kamati Kuu ni yale mazito tu.
Kuhusu mambo ya madogo yanayoishia kwenye kamati ndogo, alisema ni yale yanayoonekana yana viashiria vya majungu.
Mangula hakupatikana jana kuzungumzia majukumu ya kamati hizo lakini Makamu mwenyekiti mstaafu wa CCM, Pius Msekwa alipoulizwa kwa simu alisema majukumu na mipaka ya Kamati ya Maadili na Usalama vimeelezwa ndani ya Katiba ya CCM.
MWANANCHI
Historia inaelekea kujirudia, kama ilivyokuwa wakati Rais Jakaya Kikwete
 akizindua Bunge la 10 na wabunge wa Chadema kususia hotuba yake, ndivyo
 itakavyokuwa atakapolihutubia Bunge kwa mara ya mwisho Alhamisi bila 
kuwapo wabunge hao na wenzao kutoka NCCR – Mageuzi na CUF wanaounda 
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni (KUB).
Wabunge wa Chadema wakati huo wakiunda 
KUB peke yao, walisusia hotuba ya Rais Kikwete Novemba 30, 2010 
wakipinga matokeo ya uchaguzi uliomweka madarakani.
Safari hii wakati Rais Kikwete 
akitarajia kulihutubia Bunge hilo kwa mara ya mwisho kabla ya kulivunja 
rasmi kwa tangazo la Serikali (GN) litakalotolewa baadaye, hali 
inaelekea kuwa vilevile, lakini kutokana na sababu tofauti.
Kiongozi wa KUB, Freeman Mbowe
 alisema jana kwamba wabunge wanaounda kambi hiyo hawatahudhuria vikao 
vilivyosalia kwa sababu ya Serikali kupitisha miswada mitatu ya petroli 
na gesi kinyume cha kanuni na sheria.
“Miswada hii inahitaji umakini mkubwa kabla ya kuigeuza kuwa sheria,” alisema Mbowe na kufafanua kuwa utaratibu uliotumika utazaa sheria mbaya.
Alisema KUB na viongozi wote wa vyama 
vinavyounda Ukawa walikubaliana kuishauri Serikali, uongozi wa Bunge na 
wabunge wa CCM wasiwe na haraka katika kuipitisha miswada hiyo lakini 
hawakusikilizwa.
Mbowe alisema walikubaliana kuiacha 
miswada hiyo ipitishwe na Bunge la 11 litakaloanza Novemba ili kufanya 
uchambuzi wa kina kwa kuzingatia masilahi mapana ya Taifa.
Alisema licha ya semina mbalimbali kati 
ya wabunge wa pande mbili, kwa sababu wanazozijua wenyewe, Serikali na 
uongozi wa Bunge waliamua kuendelea kuvunja kanuni za Bunge kwa 
kupitisha miswada hiyo kwa utaratibu wa “voda fasta.”
“Tunatambua
 kuwa pamoja na maudhui mengine katika miswada hii, kuna kipengele 
muhimu ambacho kinalazimisha mikataba yote iliyosainiwa awali, ya gesi 
na mafuta, isibatilishwe.
“Mikataba
 ambayo leo hii ipo katika utekelezaji imekuwa ikilalamikiwa na watu 
wengi kuwa ina mapungufu makubwa na hivyo inalikosesha Taifa mapato 
mengi,” alisema Mbowe katika mkutano uliohudhuriwa pia na baadhi ya wabunge wa CUF na Chadema.
Alisema kwa sababu uongozi wa Bunge 
umewadhalilisha kwa kuwatoa wabunge 43 bungeni kinyume cha taratibu, ni 
dhahiri ulikusudia kuipitisha miswada yote bila kujali ushauri.
Mbowe alisema uongozi unaomaliza muda 
wake una agenda ya siri inayoufanya kulazimisha sheria hizo kupitishwa 
katika utaratibu huo.
MWANANCHI
 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, David Misime
 amewataka wageni wasiokuwa na shughuli muhimu ya kufanya mkoani hapa 
kutokuja katika kipindi cha juma hili ili kuepusha usumbufu 
utakaojitokeza.
Misime alitoa agizo hilo jana wakati 
akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake kuhusu wiki hii ambayo 
inatarajiwa kuwa na ugeni mkubwa wa wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM ambao
 amesema kuwa unakadiriwa kuwakusanya watu takribani 10,000.
Alisema ili kuepusha usumbufu 
utakaojitokeza kama vile kukosa mahali pa kulala, ni vyema kama mtu hana
 shughuli ya muhimu ya kufanya mjini hapa asije mpaka mkutano huo 
utakapokwisha.
“Kuna
 wengine wanataka kuja kwa ajili ya ushabiki tu au kuja kushuhudia tukio
 zima na hata kama hawatakuja haitawaathiri kitu hivyo ni vyema wasije 
ili kuepusha usumbufu,”  Misime.
Alisema Jeshi la Polisi limejipanga 
kuimarisha ulinzi na usalama kwa wananchi wote watakaofika katika 
mkutano huo na kuwataka wananchi kutoa taarifa za viashiria vyovyote vya
 uvunjifu wa amani katika maeneo yao.
Aliwataka wamiliki wa nyumba za kulala 
wageni kuhakikisha kuwa vitu vyote vyenye thamani vya wateja wao 
vinatunzwa vizuri ili kuepusha usumbufu au kupotea kwenye mikono yao.
Jana, Polisi waliimarisha ulinzi bungeni
 kwa kuongeza idadi ya askari na pia kufunga kipande cha barabara 
kuanzia kwenye mzunguko wa kituo kikuu cha mabasi yaendayo mikoani 
kupitia eneo la Bunge hadi mwanzo wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), 
Tawi la Dodoma.
Kulikuwa na idadi kubwa ya polisi wa 
usalama barabarani, utepe mweupe uliofungwa katika barabara hiyo huku 
kukiwekwa kibao kilichoandikwa kwa maandishi mekundu, “barabara hii 
imefungwa.”
Alipoulizwa kuhusu hatua hiyo, Kamanda 
wa Polisi Mkoa wa Dodoma, David Misime alisema kufungwa kwa barabara 
hiyo ni miongoni mwa shughuli za usalama.
NIPASHE
Wakati joto la uchujaji wa majina ya 
wagombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) likizidi kuongezeka, 
taarifa zimezidi kuzagaa mitaani na kwenye mitandao ya kijamii kwamba, 
mikakati ya kumuondoa Edward Lowassa kwenye orodha ya watia nia nayo imezidi kupamba moto.
Ofisa mmoja wa CCM makao makuu mjini 
hapa, alisema kuwa wanachofanya wao kama watendaji ni kuandaa majina ya 
wagombea wote na fomu zao za udhamini na kisha kukabidhi kwa 
sekretarieti itakayopanga ajenda za vikao vya Kamati Kuu na baadaye 
Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya taifa.
Ofisa huyo alipoulizwa kama ana taarifa 
za kuwako kwa mizengwe dhidi ya Lowassa alisema kwa ujumla kwa sasa kuna
 maneno mengi sana yanazungumzwa juu ya mchakato wa uteuzi wa mgombea, 
ila akasisitiza kuwa la msingi ni kusubiri vikao vya maamuzi.
“Ndugu yangu ukiyatazama haya makundi (ya urais) ni vigumu kuamini kama wanatoka chama kimoja. Yaani kuna kukamiana kweli kweli…Kila mmoja anataka kumwangusha mwenzake ili yeye apite,” alisema na kuongeza kuwa:
“Hata
 kama kuna mizengwe, si unajua uchaguzi huu ni wa vyama vingi. CCM 
haishindani pekee yake, kwa hiyo mgombea anayekubalika ndiye anatakiwa.”
Hata hivyo, kwa muda sasa kumekuwa na 
mfululizo wa habari za kupikwa kwamba jina la Lowassa litaishia Kamati 
Kuu kwa madai kwamba kuna ushahidi wa matumizi ya fedha kwa timu yake, 
tuhuma ambazo binafsi (Lowassa) amezikanusha mara kadhaa.
Julai mosi mwaka huu siku anarejesha 
fomu za kuwania urais kupitia CCM alitoa changamoto kwa yeyote mwenye 
ushahidi wa kuhusika kwake na rushwa ajitokeza na kusema alitoa lini, 
wapi na kwa nani.
Lowassa alisema amechoka kwa tuhuma za 
kipuuzi za kuhusishwa na rushwa na kusisitiza kuwa hakuna mwanachama 
yeyote miongoni mwa zaidi ya nane waliomdhamini aliyefanya hivyo kwa 
kishawishi cha fedha au fadhila yoyote.
Mgombea anayetajwa kutumiwa zaidi na kundi linalompinga Lowassa ni pamoja na Makongoro Nyerere, ambaye alifanya mkutano na waandishi wa habari hivi karibuni na kuporomosha kauli kali za ukakasi dhidi ya Lowassa.
Wakati mizengwe ikizidi kusukwa dhidi ya
 Lowassa, ripoti ya kura zote za maoni ambazo zimekuwa zikitolewa katika
 miezi ya hivi karibuni zimeonyesha kuwa Lowassa anaongoza kwa mbali 
kama chaguo la wananchi wengi kwenye nafasi hiyo.
Miongoni mwa tafiti hizo ni ule wa 
Mpango wa Utafiti na Elimu ya Demokrasia (REDET) ya Chuo Kikuu cha Dar 
es Salaam, uliofanywa mwezi uliopita na matokeo yake kutolewa mwishoni 
mwa wiki unaonyesha kuwa Lowassa ni changuo la kwanza la wengi kwa 
kujipatia asilimia 27.0 ndani ya chama hicho, huku Bernard Membe 
akishikilia nafasi ya pili kwa kupata asilimia 8.2.
Katika utafiti huo ambao REDET walisema 
kuwa unaweza kuchukuliwa kwa ujumla wake kama maoni ya Watanzania endapo
 masuala yaliyoulizwa uchaguzi ungefanyika katika kipindi cha utafiti, 
wahojiwa walikuwa 1,250 kutoka wilaya moja moja katika mikoa 25 ya 
Tanzania Bara.
Wakati mkakati wa mizengwe ukiendelea 
kupamba moto, wajumbe wa sekretarieti ya Kamati Kuu ya chama hicho 
wanaanza vikao mjini hapa leo kundaa pamoja na mambo mengine ajenda na 
taarifa kwenye vikao vya Kamati Kuu itakayokaa Alhamisi mjini hapa.
Kikao cha Kamati Kuu kinatarajiwa 
kuchuka majina ya watia nia 38 waliojitokeza kutafuta ridhaa ya chama 
hicho na kubakisha majina matano tu yatakayopelekwa NEC kwa kupigiwa 
kura.
NEC inayotarajiwa kukutana Ijumaa wiki 
hii, itatoa majina matatu kwenda Mkutano Mkuu unaotarajiwa kukutana 
Jumamosi kwa ajili ya kupata jina moja la mgombea urais wa CCM katika 
uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu.
NIPASHE
Tume ya uchaguzi Zanzibar (ZEC) imeongeza majimbo ya uchaguzi kwa Zanzibar kutoka 50 hadi 54.
Hata hivyo, majimbo yaliyoongezwa ni ya upande wa Unguja wakati Pemba imeendelea kuwa na majimbo 18 kama ilivyokuwa awali.
Hatua hiyo ya Zec kuongeza majimbo ya 
uchaguzi inatokana na tume hiyo kupewa mamlaka ya kuchunguza mipaka na 
majimbo ya uchaguzi na baada ya uchunguzi inaweza kubadili idadi, mipaka
 na majina ya majimbo kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.
Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari 
visiwani hapa kuhusiana na mabadiliko ya idadi, mipaka na majina ya 
majimbo ya uchaguzi jana, Mwenyekiti wa Zec, Jecha Salum Jecha, alisema tume hiyo imetumia vigezo na maoni ya wadau wa uchaguzi vikiwamo vyama vya siasa katika ugawaji wa mipaka ya majimbo.
Jecha alisema tume hiyo pia katika 
ugawaji huo imezingatia idadi ya watu na zaidi katika kuhakikisha 
uwakilishi unaofaa katika miji mikubwa na miji ya mashamba yenye idadi 
ndogo ya watu, njia za usafiri na mipaka ya sehemu ya utawala.
Majimbo mapya yaliongozeka kwa upande wa Unguja katika wilaya ya Magharibi ni Chukwani, Pangawe, Kijitoupele na Welezo.
Aliyataja majina mapya ya majimbo kwa 
Unguja kuwa ni Mahonda, Kiwengwa, Kijini, Tunguu, Paje, Shaurimoyo, 
Malindi, Mtopepo na kwa upande wa Pemba ni jimbo la Wingi.
Utaratibu huo wa tume ya uchaguzi 
umefanya Unguja kuwa na majimbo 36 ambapo awali kulikuwa na majimbo 32 
na kisiwani Pemba idadi ni ileile ya wali ya majimbo 18.
Majina ya majimbo ya awali ambayo kwa 
sasa hayatatumika tena ni jimbo la Kitope ambalo linashikiliwa na Makamu
 wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi, kwa nafasi ya ubunge. Mengine ni
 la Rahaleo, Mjimkongwe, Magogoni, Mkanyageni, Matemwe, Muyuni na Koani.
 Kaimu Mkurugenzi wa Habari na 
Mawasiliano wa Chama cha Wananchi (CUF), Ismail Jussa Ladhu, alisema 
chama hicho kimepokea kwa furaha kubwa sana taarifa ya tume hiyo ya 
mapitio ya majimbo kutoka majimbo 50 ya sasa hadi 54.
“Ushindi
 katika uchaguzi mkuu unapatikana kwa wananchi kujiandikisha na kwenda 
kupiga kura, sio ukataji wa majimbo kwani mkato huo wa mipaka ya majimbo
 umeturahisishia sana kazi ya kushinda katika uchaguzi mkuu,” Jussa.
Jussa ambaye pia ni mwakilishi wa Jimbo 
la Mjimkogwe ambalo sasa litakuwa ni jimbo la Malindi, alisema licha ya 
tume hiyo kumaliza kazi ya mapitio ya majimbo, lakini haikuzingatia 
maoni ya wadau na badala yake imejiamulia kuongeza majimbo wakati 
hakukuwa na sababu ya kuongeza majimbo hayo.
Alisema: “Tume haijazingatia mipaka ya utawala, idadi ya watu katika miji mikubwa ya mijini na miji midogo ya shamba.”
Hata hivyo, alisema licha ya tume hiyo 
kuamua kuongeza majimbo 54, lakini bado CUF kina uhakika wa kushinda 
majimbo 34 ya uchaguzi katika uchaguzi mkuu na kuigaragaza CCM.
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibae, Vuai 
Ali Vuai, alisema wameridhika na maamuzi ya tume kuongeza majimbo manne,
 lakini akaeleza kuwa tume hiyo haikutenda haki kwa majimbo ya Pemba.
Alisema kuwa kwa mujibu wa idadi ya watu
 iliyopo Pemba, ilipaswa tume hiyo kupunguza majimbo kisiwani humo 
badala ya majimbo 18, yawe majimbo 16.
“Licha ya tume kuamua, lakini sisi hatuna pingamizi na tume hiyo kwa sababu tume hiyo ndio waamuzi,” alisema Vuai.
Alisema CCM itaanza kutoa fomu za 
kuwania ubunge, udiwani na uwakilishi kuanzia Julai 15 na  ana imani 
kubwa kuwa CCM itashinda kwa kishindo kikubwa katika uchaguzi huo 
unaotarajiwa kufanyika mwishoni mwa Oktoba, mwaka huu.
Ali Makame kutoka chama cha ACT 
Wazalendo, alisema chama hicho kimepokea kwa hisia nzuri maamuzi hayo ya
 Zec kutokana na uwezo waliopewa.
“Licha ya taarifa hiyo ya tume ya 
uchaguzi kuongeza majimbo 54, lakini haki haikutumika kama 
tulivyotegemea kwani baadhi ya majimbo tumeona kuwa na shehia nyingi na 
baadhi kuwa na shehia kidogo,” alisema Makame.
Aidha, alisema kwa kuwa hakuna sheria 
inayoruhusu kuwa na pingamizi kutokana na maamuzi ya tume hiyo katika 
uchunguzi na ugawaji wa majimbo, inabidi wakubali matokeo.
Zec ilianza kazi ya uchunguzi wa idadi, 
mipaka na majina ya majimbo ya uchaguzi Juni 9, mwaka 2014 kwa kupokea 
na kusikiliza maoni ya wadau wa uchaguzi kwa mujibu wa kifungu cha 
120(3) ya Katiba ya Zanzibar.
Kabla ya tume hiyo kufanya kazi hiyo na 
kuamua kuongeza majimbo 54 kutoka 50 kazi kama hiyo ilifanyika mwaka 
2004 na Pemba ilipunguzwa majimbo matatu na kuwa na majimbo 18 kutoka ya
 awali 21 na Unguja ikaongezewa majimbo mawili kutoka majimbo 29 ya 
awali.
NIPASHE
Chama cha Wananchi (CUF), kimesema 
kitaitisha maandamano kwenye mikoa yenye gesi ili kulishinikiza Bunge 
kupinga muswada wa mafuta na gesi uliopitishwa juzi.
Akihutubia wakazi wa Manispaa ya Kigoma/Ujiji na viunga vyake, Mwenyekiti wa Taifa wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, alisema haoni mantiki na hakuna sababu ya kufanya haraka kupitisha muswada huo.
“Suala
 hili linahitaji mjadala wa kina utaohusisha wadau mbali mbali, 
wataalamu na wananchi kwa ujumla wake,” alisema Profesa Lipumba na 
kuongeza:
“CUF
 inaunga mkono jitihada za wabunge wa kambi ya upinzani kwa hatua zao 
kupinga muswada huo, ambao haukujali na wala haukuzingatia maslahi ya 
Taifa.”
Alisema CUF inatoa angalizo kwa Rais 
Jakaya Kikwete kwamba kwa hali inavyoenda huenda akaenda kufunga Bunge 
litalokuwa na Wabunge wa CCM pekee.
“Hiyo
 inatokana na ukweli kwamba Spika wa Bunge amepoteza muelekeo na 
ameshindwa kabisa kuliongoza Bunge kwa mujibu wa kanuni walizojiwekea 
katika kutimiza wajibu,” alisema Profesa Lipumba na kuongeza:
“Kwa hiyo  basi, Rais Kikwete atakuwa amefuata nyayo za Rais wa Zanzibar.”
Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein 
Juni 26, mwaka huu alilivunja Baraza la Wawakilishi bila Wawakilishi wa 
CUF kuwapo barazani.
Wajumbe hao walisusia Baraza hilo 
kutokana na kutoridhishwa na uandikishaji wa wapigakura katima daftari 
la kudumu la wapigakura kwa kutumia mfumo wa kielektroniki unaojulikana 
kama Biometric Voters Registrarion (BVR), wakisema kuwa uandikishaji huo
 ulitawaliwa na ubabe.
Profesa Lipumba alionya kuwa kama Bunge litaendelea na mpango wake huo, basi CUF  ataitisha maandamano ili kupinga muswada huo.
Katika hatua nyingine, Profesa Lipumba 
alisema kuwa Mkoa wa Kigoma unaweza kuendelea kiuchumi ikiwa utatumia 
vizuri rasilimali zilizoko akitolea mfano Hifadhi ya Taifa ya Gombe 
kwamba ikitumika vizuri inaweza kuingiza mapato mengi.
Alisema kwamba jiografia ya Mkoa wa 
Kigoma inauruhusu kupata fursa nyingi za kuendelea kiuchumi kwa kuwa 
wananchi wake wanaweza kufanya biashara na nchi zinazouzunguka za 
Burundi Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
HABARILEO
Vilio na simanzi vilitawala katika eneo la mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu baada ya Waziri wa zamani wa Fedha, Basil Mramba na Waziri wa zamani wa Nishati na Madini, Daniel Yona, kuhukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela.
Wake wa Mramba na Yona na waliodaiwa 
kuwa ni watoto wao walionekana wakilia kila wakati mahakamani hapo, huku
 ndugu, jamaa na marafiki wakiwa wanawabembeleza na kuwaambia wamuachie 
Mungu.
Hata hivyo, baadhi ya ndugu jamaa na marafiki wa aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Gray Mgonja, walionekana kuwa na furaha baada ya mahakama kumwachia huru.
Washtakiwa hao wamehukumiwa baada ya 
kupatikana na mashitaka ya matumizi mabaya ya madaraka na kuisababishia 
serikali hasara ya Sh bilioni 11.7 yaliyokuwa yanawakabili wote watatu.
Hukumu hiyo ilitolewa jana na Jopo la 
Mahakimu watatu likiongozwa na Hakimu John Utamwa, mahakimu wengine ni 
Sam Rumanyika na Saul Kinemela.
Akisoma hukumu hiyo iliyowahi 
kuahirishwa mara mbili, Hakimu Rumanyika alisema Mramba amepatikana na 
hatia ya mashitaka 11 na Yona kwa mashitaka matano.
Katika adhabu ya Mramba, Hakimu 
Rumanyika alisema, kuanzia kosa la kwanza hadi la kumi linalohusu 
matumizi mabaya ya Ofisi kinyume cha sheria, anahukumiwa kifungo cha 
miaka mitatu jela na haina masharti ya kulipa faini.
Katika shitaka la 11 la kuisababishia 
serikali hasara ya Sh bilioni 11.7, alisema Mramba anatakiwa kulipa 
faini ya Sh milioni tano au kutumikia kifungo cha miaka mitatu jela.
Kuhusu Yona, Hakimu Rumanyika alisema 
anahukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela baada ya kupatikana na hatia 
ya mashitaka matano kati ya 11 yaliyokuwa yanamkabili.
Alisema amepatikana na hatia ya matumizi
 mabaya ya Ofisi ikiwa ni kinyume cha sheria, hivyo anahukumiwa kifungo 
cha miaka mitatu jela aidha mashitaka ya kuisababishia serikali hasara 
ya fedha hizo, atatumikia kifungo cha miaka mitatu jela au kulipa faini 
ya Sh milioni tano.
Akiendelea kusoma hukumu hiyo, Hakimu Rumanyika alisema, Mgonja hajapatikana na hatia yoyote, hivyo Mahakama inamuachia huru.
Baada ya kusoma hukumu hiyo kwa zaidi ya
 saa moja na nusu, Mramba na Yona waliwekwa chini ya ulinzi wa Jeshi la 
Magereza kabla hawajashuka kizimbani huku baadhi ya ndugu waliofika 
mahakamani wakiangua kilio na ndugu wa Mgonja wakiwa na furaha huku 
wakimshukuru Mungu.
Katika kesi hiyo washitakiwa walikuwa 
wanakabiliwa na mashitaka 11, mashitaka 10 yanahusu Matumizi mabaya ya 
madaraka na moja la kuisababishia Serikali hasara ya Sh bilioni 11.7.
Upande wa Jamhuri uliita mashahidi saba 
kuthibitisha kesi hiyo ambapo Mahakama iliwaona washtakiwa wana kesi ya 
kujibu na katika utetezi wao washitakiwa walijitetea wenyewe na kuita 
mashahidi wawili.
Kwa mara ya kwanza washitakiwa 
walifikishwa mahakamani hapo mwaka 2008 ikiwa ni miaka saba iliyopita, 
wakikabiliwa na mashitaka ya kuisababishia Serikali hasara ya kiasi 
hicho kutokana na msamaha wa kodi kwa Kampuni ya kukagua madini ya 
dhahabau ya M/S Alex Stewart ya Uingereza.
Katika utetezi wake Mramba alikiri 
kuisamehe kodi kampuni hiyo kwa kuwa kulikuwa na mkataba uliosainiwa 
Juni 2003 kati ya Kampuni hiyo na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ambao 
ulikuwa unaonesha malipo yafanyike bila ya kukatwa kodi.
Hata hivyo upande wa Jamhuri ulidai, 
msamaha huo ulitolewa wakati tayari Wizara ilikuwa imepokea barua za 
kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ambazo zilikuwa zinakataa 
kampuni hiyo isisamehewe kodi.
BONYEZA HAPO UONE VIDEO YA MTOTO MKALI;
Ugandan socialite Zari is undeniably hot and Diamond Platnumz cannot be blamed for going kookoo for her, Besides her looks, she is also ambitious and rich.
Born on 23rd of September 1980, Zari grew up in Jinja and after high school she moved Kampala where she performed karaoke in hang-outs. She later moved to London and acquired a diploma in cosmetology.
She now lives in South Africa where she runs cosmetics shop while pursuing a career in music.
She shared some of her never before seen photos from back in the day and she was still hot.


 
 
 
 
 
 
Post a Comment